KUWAONA STARS, MSUMBIJI KIINGILIO BUKU 7,000/- VITI MAALUM (VIP) 30,000/-

Viingilio kwa mechi ya Taifa Stars na Msumbiji itakayochezwa keshokutwa (Jumapili) Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ni sh. 7,000 na sh. 30,000 kwa viti maalumu 4,500 tu.

Kuanzia kesho asubuhi (Jumamosi) tiketi za kielektroniki zitauzwa pia katika magari maalumu kwenye vituo vya Buguruni Shell, Dar Live Mbagala, Ferry Magogoni, Kigamboni, OilCom Chang’ombe, OilCom Ubungo, Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa (Kariakoo), TCC Club Chang’ombe na Uwanja wa Taifa.

Aidha tiketi zinapatikana kupitia M-PESA kwa kupiga *150*00# kisha bonyeza 4,  bonyeza tena 4 kisha weka namba ya kampuni 173399 kisha ingiza 7000 kama namba ya kumbukumbu ya malipo, kisha andika tena 7000 kwenye weka kiasi, kasha weka namba ya siri na baadaye bonyeza  1 kukubali.

Utapokea ujumbe wenye orodha ya vituo vya MaxMalipo vya kuchukua tiketi ukiwa na namba ya uhakiki wa malipo yako.

Vituo vya MaxMalipo vya kuchukulia tiketi ni mgahawa wa Steers uliopo mtaa wa Samora/Ohio, maduka makubwa ya Uchumi Supermarket (Quality Centre, Tabata Segerea na kituo cha daladala Makumbusho), Sheer Illussions (Millennium Tower na Mlimani City), maduka makubwa ya TSN Supermarket (City Centre, Kibo Tegeta na Upanga).



Vodashop (Ubungo na Mill Pamba), Shop Mwenge (Born to Shine), Puma Petrol Station (Mwenge na Uwanja wa Ndege), Engen Petrol Station (Mbezi Beach), Big Bon Petrol Station (Kariakoo, Sinza Mori, Mbagala na Temeke), YMCA (Posta Mpya), City Sports Lounge (Posta), Uwanja wa Taifa) na Uwanja wa Karume.

Akizungumza nawaandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij, alitaja Kikosi kitakachoiwakilisha Tanzania kuwa ni, makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Aishi Manula, mabeki Said Mourad, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Aggrey Morris, Kevin Yondan na Edward Charles, wakati viungo ni Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Shaaban Nditi, Simon Msuva, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Khamis Mcha, Ramadhani Singano ‘Messi’, Haroun Chanongo, Amri Kiemba na washambuliaji Mrisho Ngassa, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na John Bocco.
 
Kwa upande wa Nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema kwamba anaomba Watanzania wajitokeze kwa wingi Uwanja wa taifa mjini Dar es Salaam kuisapoti timu yao.



“Tunashukuru hadi kufika hapa, ni matunda ya kupambana kwa juhudi na pia sapoti yenu, kwa hivyo tunaomba muendelee kuwa nasi Jumapili, watu waje kwa wingi wasapoti timu, ifanya vizuri,”amesema Cannavaro.



Aidha nahodha huyo wa taifa Stars amesema bado ana kumbukumbu za kipigo walichokipata dhidi ya Msumbiji mwaka 2007,wakati Nooij akiwa kocha mkuu wa Mambas,  na kwa maana hiyo hivi sasa akiwa chini yake atafanya kila juhudi kwa faida ya Watanzania na yeye mwenyewe binafsi.


Stars itamenyana na Msumbiji Jumapili katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mwisho wa mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya AFCON mwakani nchini Morocco, ambao kiingilio cha chini kitakuwa Sh. 7,000.

0 comments:

Post a Comment