Mwanamke aliyeiba Mtoto huko Sumbawanga ili kulinda Ndoa Yake Ahukumiwa Mwaka mmoja Jela

Mkazi wa kijiji cha Kisumba, Manispaa ya
Sumbawanga, Halima Nambeya (18)
ametupwa jela mwaka mmoja na
Mahakama ya wilaya ya Sumbawanga
baada ya kukiri kosa la kuiba mtoto
mchanga wa kiume kwa lengo la kulinda
ndoa yake ili asiachike kwa kukosa mtoto.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa,
Frednand Rwegasira alisema mtuhumiwa
huyo alimuiba mtoto huyo katika eneo la
Jangwani mjini hapa na kumsafirisha hadi
kijijini Kisumba nyumbani kwa babu yake.
"Halima alifikishwa mahakamani na
kusomewa mashitaka ya wizi wa mtoto
na alikiri kosa lake hilo na amehukumiwa
kutumikia kifungo cha mwaka mmoja
jela," alisema.
"Uchunguzi wa awali ulibainisha kuwa
Halima awali alimdanganya mumewe
alikuwa mjamzito hivyo anadaiwa
kumuiba mtoto huyo mchanga ili
amdanganye mumewe kuwa amejifungua
kwa lengo la kulinda ndoa yake ili
asiachike," alibainisha Kaimu Kamanda
huyo.
Kwa mujibu wa Rwegarisa, Halima
anadaiwa kutenda kosa hilo Juni 29
mwaka huu ambapo alikamatwa na Polisi
siku nne baadaye akiwa nyumbani kwa
babu yake kijijini Kisumba, Manispaa ya
Sumbawanga.

0 comments:

Post a Comment