RAGE AIKABIDHI RASMI SIMBA SC KWA AVEVA, LAKINI MAMBO YA FEDHA ‘AYAKWEPA KIDOGO’

ALIYEKUWA mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage jana alikabidhi ofisi kwa Rais mpya wa klabu hiyo, Evans Aveva lakini alishindwa kuweka wazi fedha ambazo anaziacha kwenye akaunti ya klabu hiyo.
Gazeti la Nipashe la leo limeandika kwamba, Rage alisema kuwa masuala ya pesa yanahitaji mambo mengi ya kiufundi hivyo atatangaza baadae masuala yote ya pesa.
"Nina imani kubwa na uongozi huu, ninakabidhi kila kitu kwa uongozi mpya lakini suala la akaunti na pesa zilizopo ni suala ambalo nitakaa na uongozi na kuwakabidhi baada ya kukamilisha baadhi ya mambo," alisema Rage.
Kutoka kulia walioketi, Alhaj Rage, Aveva na Ezekiel Kamwaga Katibu wa klabu, wakati nyuma waliosimama kutoka kulia ni Iddi Kajuna, Said Tuliy na Jasmin Badour, wote Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wakati wa makabidhiano jana Msimbazi

Rage jana alikabidhi nyaraka mbalimbali kwa uongozi mpya ikiwemo mikataba ya wachezaji na klabu hiyo pamoja na mikataba ya wafanyakazi wengine.
Pia alikabidhi jengo la klabu hiyo na mikataba ya wapangaji pamoja na nyaraka za uwanja wao wa Bunju. pia alikabidhi katiba ya klabu hiyo pamoja na katiba ya Shirikisho la soka nchini (TFF).
Rage alikabidhi vitu hivyo huku akitaka klabu hiyo kuwa na umoja utakaowasaidia kufanya vizuri kwenye mashindano ya ndani pamoja na yale ya kimataifa.
"Nakuomba Rais Aveva, kuimarisha umoja wa klabu pamoja na kuvunja makundi yote, ni vizuri ukakaa pamoja na wanachama waliofungua kesi mahakamani ili kupata suluhu," alisema Rage
Kwa upande wake, Aveva alimshukuru Rage na kusema kuwa ni kiongozi aliyeonyesha moyo wa upendo na kuwasaidia wakiwa kama viongozi wapya wa klabu hiyo.
Alisema kuwa uongozi wa rage ulifanya kazi kubwa na ulikuwa na malengo ya kuhakikisha timu inakuwa katika nafasi nzuri huku wakiwa na mipango mizuri.
Alisema kuwa uongozi wake utaendeleza mambo yote mazuri ambayo uongozi wa rage uliyafanya ili kuhakikisha timu inakuwa katika nafasi nzuri nje na ndani ya uwanja.


0 comments:

Post a Comment